Mojawapo ya vigezo vinavyozingatiwa wakati wa usajili wa
wanafunzi katika taaluma za uanahabari ni ukwasi wa lugha. Taasisi nyingi
nchini Kenya zinazotoa mafunzo hayo katika viwango mbali mbali vikiwemo
shahada, diploma na vyeti hususani katika utangazaji hupendelea wanafunzi waliofanya
vizuri katika somo la Kiingereza, Kiswahili au yote mawili.
Sababu ya kufanya hivyo ni kuhakikisha wanafunzi hao ambao
ni wataalamu wa badaye wana uwezo wa kujieleza kwa lugha yoyote kati ya hizo mbili
za kitaifa iwe ni kwenye magazeti, majarida, redio, runinga au hata mtandaoni.
Jukumu kubwa zaidi la mwanahabari ni kuwasilisha ujumbe kwa hadhira na ni
dhahiri kwamba ala muhimu anayohitaji kufanyia hivyo ni lugha.
Hapo awali, kulingana na katiba, lugha ya Kiingereza
ilitambulika kama lugha ya kitaifa ilhali ile ya Kiswahili ikasemekana kuwa ni
lugha rasmi. Hata hivyo, kulingana na katiba mpya iliyoidhinishwa kupitia kura
ya maoni ya mwaka wa 2010, Kiswahili pia kinatambulika kama lugha ya kitaifa na
inachukuliwa kwa usawa na Kiingereza.
Cha kushangaza ni kwamba lugha ya Kiswahili haijatiliwa
mkazo katika kuwafunza wanaodhamiria kuwa watangazaji katika baadhi ya vyuo
vikuu na vyuo anuai. Mfano mzuri ni chuo kikuu cha Moi, kinachotoa mafunzo
tofauti tofauti yanayohusiana na utangazaji. Katika kitivo cha sayansi za
habari, kunayo taaluma ya sayansi ya uanahabari. Kati ya jumla ya masomo 56
anayofaa kuyapitia mwanafunzi kabla ahitimu, mawili tu ndiyo hufunzwa kwa lugha
ya Kiswahili.
Hali hii imesababisha wanafunzi wengi kutoimarika katika
kuandika au kuzungumza kwa lugha ya Kiswahili, jambo ambalo huathiri utendakazi
wao hasa wale wanaoajiriwa katika vyumba vya habari vinavyotangaza au kuandika
kwa Kiswahili. Wanapolazimika kuitumia lugha hiyo, hufanya hivyo wakiwa na
mtazamo hasi au bila kuzingatia usahihi wa kisarufi. Wanahabari hao mara nyingi
hushindwa na tafsiri za maneno ya kimsingi hivyo basi hutumia njia ya mkato ya
kutohoa misamiati mingi kutoka kwa lugha zengine.
Kuna haja ya taasisi mbali mbali kufanya mageuzi katika
mtaala wao, si katika taaluza za utangazaji tu bali na nyenginezo pia. Mtu
anayesomea kozi ya kibiashara kwa mfano, anayeazimia kufanya kazi kama
mkurugenzi wa kampuni, ni muhimu ajue kuwasiliana kwa lugha ya Kiswahili kando
na ya Kiingereza, na si Kiswahili tu bali Kiswahili sanifu.

No comments:
Post a Comment