Shirikisho
la kandanda nchini Kenya FKF limeteua wanachama wapya wa kamati ya kiufundi ya
timu ya taifa Harambee Stars.
Akihutubia
wanahabari hapo jana katika hoteli moja jijini Nairobi, mwenyekiti wa FKF Bw.
Sam Nyamweya alimtaja (aliyekuwa) kocha wa klabu ya Gor Mahia Bobby Williamson
kama mkufunzi mpya wa Harambee Stars. Nahodha wa zamani wa timu hiyo Musa
Otieno ndiye kocha msaidizi huku Simon Muluma akikabidhiwa wadhifa wa meneja
mkurugenzi.
Hatua
hii imeafikiwa siku mbili tu baada ya raia wa Ubelgiji Adel Amrouche kutimuliwa
kama kocha wa Harambee Stars kufuatia matokeo duni ya timu hiyo. Amrouche
pamoja na wanakamati wote wa kiufundi waliachishwa kazi siku ya Jumapili, muda
mchache tu baada ya timu hiyo ya taifa kupoteza nafasi ya kufuzu kwa michuano
ya taifa bingwa barani Afrika. Timu hiyo ilitoka sare tasa na timu ya taifa ya
Lesotho katika mechi ya marudio baada ya kupoteza 1-0 hapo awali kwenye mechi
ya kwanza.
Bobby
Williamson alikuwa mkufunzi wa timu ya taifa ya Uganda, Uganda Cranes, kwa muda
wa miaka mitano kabla ya kuteuliwa kusimamia Gor Mahia mnamo Julai mwaka jana.
Katika msimu wake wa kwanza, Williamson aliiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa
ligi kuu nchini Kenya.
