Gor Mahia yaaga mashindano
Klabu ya Gor Mahia iliyowakilisha
Kenya katika michuano ya CECAFA Kagame Cup nchini Rwanda ilibanduliwa mapema
baada ya kulazimishwa sare ya mabao 2-2 na APR siku ya Jumamosi. Gor
ilihitajika kushinda mechi hiyo ili kufufua matumaini ya kusalia katika
mashindano hayo baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza katika hatua ya
makundi.
Gor Mahia ilicheza mechi yake ya mwisho jana jioni dhidi ya Telecom ya Djibout, mechi ambayo matokeo yake hayangeathiri popote kwani timu zote mbili tayari zilikuwa zimepoteza nafasi ya kufuzu kwa hatua ya muondoano.
Gor ilifedheheka kwa kushika mkia
katika kundi B baada ya kuvuna alama mbili tu ndani ya mechi nne. Inatarajiwa
kurejea nyumbani hii leo ili iendeleze kibarua cha kutetea taji ya ligi kuu ya
Premier nchini, dhidi ya SoNy Sugar siku ya Jumapili.
Manchester United yaanza kwa kichapo
Vigogo wa Wingereza Manchester United walianza msimu mpya wa
ligi kuu ya Premier nchini humo kwa mshangao baada ya kuchapwa mabao 2-1 na
Swansea City uwanjani kwao Old Trafford siku ya Jumamosi.
Chini ya mkufunzi mpya Louis van
Gaal, United waliingia uwanjani wakiwa na matumaini makubwa hasa baada ya
kushinda mechi zao zote sita za matayarisho ya msimu dhidi ya La Galaxy, AS Roma,
Inter Milan, Real Madrid, Liverpool na Valencia katika usanjari huo.
Hata hivyo dau lilianza kwenda
mrama wakati raia wa Korea Sung-Yueng Ki alipoiweka Swansea kifua mbele mnamo
dakika ya 28 ya mchezo. Muda mfupi baada ya mapumziko, nahodha mpya wa Mancheter
United Wayne Rooney alisawazishwa kwa bao la mtindo wa pindu kabla Gylfi
Sigurdsson kuipa Swansea bao la ushindi, dakika 18 kabla mechi kutamatika. Hiyo
ilikuwa mara ya kwanza United kupoteza mechi ya ufunguzi wa msimu wakiwa
nyumbani tangu mwaka wa 1972.
Kwa upande wao Arsenal waliponyoka na ushindi wa mabao
2-1 dhidi ya Crystal Palace nyumbani kwao Emirates, kwa hisani ya mabao ya
Laurent Koscielny na Aaron Ramsey waliyoyafunga katika muda wa ziada wa kipindi
cha kwanza na cha pili mtawalia.
Kwengineko chipukizi wa Wingereza
Raheem Sterling na Daniel Sturridge walisaidia Liverpool kuandikisha ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Southampton
jana jioni, kabla Manchester City kuilaza
Newcastle kwa mabao 2-0 kupitia mickwaju ya David Silva na Sergio Aguero.
Hivi leo Chelsea watakuwa ugenini dhidi ya timu iliyopandishwa daraja
msimu-jana Burnley katika mechi iliyoratibiwa kuanza saa nne kamili usiku.
Je, wajua?
Toni Kroos ameshinda makombe 4
katika mechi 10 za mwisho alizoshiriki!
|
Tarehe
|
Kombe
|
Timu
|
|
11/5/2014
|
Bundesliga
|
Bayern
|
|
17/5/2014
|
DFB Pokal
|
Bayern (dhidi ya Borussia Dortmund)
|
|
13/7/2014
|
Kombe la dunia
|
Ujerumani (dhidi ya Argentina)
|
|
12/8/2014
|
UEFA Super Cup
|
Real Madrid (dhidi ya Sevilla)
|
