Je, uliposajiliwa kama mwanafunzi katika bewa kuu la
chuo kikuu cha Moi, ilikuwa mara yako ya ngapi kukanyaga ardhi ya mahala hapa?
Swali hili, katu haliwezi kuzalisha majibu sawa kwa wadau tofauti tofauti katika
taasisi hii ya elimu.
Kunao waliowahi
kuzuru mahali hapa hata kabla hawajajua kwamba huenda hatimaye wakajipata papa
hapa katika safari yao ya kutafuta shahada.
Aidha kuna wale ambao, mimi nikiwa mmoja wao, waliyaona
mandthari ya Moi mara ya mosi katika pilkapilka za kusajiliwa kiuanagenzi.
Kwa wanafunzi wa shule ya upili ua St. Teresa’s
Opanga - iliyoko eneo la Kadongo katika mkoa wa Nyanza, hii leo imekuwa siku njema kwa
baadhi yao waliopata nafasi ya kuzuru chuo hiki. Kwa hakika hii ni hatua
kabambe sana, hasa tukizingatia saikolojia ya mwanadamu – ambaye hupata mvuto
wa kukienzi kitu anachokiona kwa macho kuwa kizuri. Natumai kunao wengine ambao
tayari wamepata motisha utakaowatia ngoa na kuwapa msukumo wa kufanya vyema
katika mtihani wao wa kitaifa wa KCSE, ili mwisho wa siku nao wajivunie kuwa
wana-Moi au chuo kikuu chochote chenginecho.![]() |
| Wanafunzi wa Teresa's - Chuoni Moi |
Dhana ya kwamba wanafunzi hao wamependezewa na
mahali hapa ungeithibitisha tu, kama ungepita karibu nao na kutazama tabasamu
lililokuwa limetanda nyusoni mwa wengi wao – kama si wote. Wengine hawakutaka
kuondoka kisha waisahau siku hii maishani mwao, hivyo basi wakaamua kupiga
picha katika maeneo fulani fulani yaliyoonekana kuwavutia zaidi. Wanafunzi hao
wametembezwa sehemu mbali mbali zikiwemo ukumbi wa wanafunzi, maktaba, kitivo
cha rasilimali-watu, afisi za utawala na kadhalika.
Lakini kwa kauli yangu, wanafunzi hao wameikosa
fursa ya dhahabu, ambayo ingewapa taswira kamili ya maisha chuoni humu, kwa
kutopelekwa sehemu nyeti kama vile hosteli H na J. Huko, wangejionea maajabu ya
mwaka na hata pengine kuchanganyikiwa kwa taarifa-kinzani. Huku muelekezi wao akisema,
“Hapa ni H, hosteli inayoishi wanafunzi wa kiume tu…” wakati huo huo anatokezea
binti mmoja au wawili wakitoka kuoga na wanaingia ‘vyumbani mwao’. Huko J pia,
muelekezi angesema, “Humu ni mwa wasichana sasa…” mara ghafla wanakutana na
barobaro limeshikilia kifuko cha ngumuu na linafungua mlango wa ‘chumba chake’!
Hata hivyo, waliyoyapata yanatosha, kwani wanafunzi
hao wamejifunza mengi kwa kujionea, kujisomea na hata kwa kusikia pia; hayo
yote ni katika fursa waliyopewa, fursa ya kutamanika – Fursa niliyoikosa!!!


No comments:
Post a Comment