Wanafunzi
hao walibeba matawi huku wakiimba wimbo wa mapambano na kufululiza hadi katika
afisi za usimamizi wa chuo ili kueleza kutoridhika kwao. Walitaka kuhutubiwa na
Naibu wa Chansela Bw. Richard Mibey, lakini badala yake akawatuma wasaidizi
wake wawili kuwatuliza waandamanaji kwa kuwahakikishia kwamba tatizo hilo sugu
lingetatuliwa mara moja.
Haikuwa
kazi rahisi kwa wawili hao kuzima ghasia hizo hadi mwishowe wakawasiliana na
mkurugenzi wa kampuni ya Kenya Power tawi la Eldoret ili afike chuoni humo mara
moja. Alipowalisi, mkurugenzi huyo, ambaye alikosa hata nafasi ya
kujitambulisha kwa jina, alilazimika kuvumilia matusi na kelele kutoka kwa
wanafunzi waliojawa na hasira, kabla hatimaye kutoa hotuba yake kwa kifupi.
“Tayari
chuo chenu kimelipa pesa kwa kampuni ya Kenya Power, kwa hivyo kesho asubuhi
wafanyikazi wetu watakuwa hapa ili kutatua tatizo hili. Tutaweka mashini mpya
ya kudhibiti na kusambaza umeme, shughuli itakayotuchukua siku moja au mbili
kuanzia kesho.”
Hotuba
hiyo ilisaidia pakubwa katika kutuliza ghasia hizo na hali ya utulivu ikarudi
tena chuoni humo, na shughuli nyenginezo zikandelea.
Hata
hivyo, mwendo wa saa moja jioni, ghasia hizo zilizuka upya baada ya umeme kutoweka
tena na hapo ndipo wanabiashara walihesabu hasara.
Kwa
kisingizio cha njaa, wanafunzi hao walivamia soko la mboga na matunda na kuanza
kupora chochote chenye ladha ya chakula. Sukuma, kabeji, nyanya, vitunguu,
ndizi, parachichi, na kadhalika, wanafunzi walijishindia. Hata vibanda vya soko
hilo pia vilikiona cha mtema kuni kwani viligeuzwa maghofu kwa muda usiozidi
nusu saa.
Duka
la kuuzia vibanzi, chapi na mahamri lililo karibu pia halikusamehewa, kwani pia
lilisaidia kukata njaa ya waandamanaji hao. Baadaye walivamia duka lengine mita
kadhaa kutoka hapo na kupora chochote kilichokuwa ndani baada ya kufanikiwa
kuvunja milango na madirisha.
Hii
leo mwendo wa saa tatu gari la kampuni ya Kenya Power limewasili chuoni pamoja
na wahandisi na vifaa vyao ili kuanza shughuli ya kurekebisha hitilafu za umeme
kwa lengo la kuzuia ghasia kama hizo kutokea tena siku za usoni.

No comments:
Post a Comment