Chama cha Msalaba Mwekundu cha
wanafunzi wa chuo kikuu cha Moi, hapo juzi Jumamosi tarehe 26 mwezi Julai
kilizindua rasmi mpango wa kuyarembesha mazingira.
![]() |
| Baadhi ya wanachama wakipanda miche |
Moja wapo ya mikakati
waliyoitumia ni kuandaa msafara ulioanzia nje ya jumba la ukumbi wa wanafunzi,
chini ya uongozi wa mwenyekiti wa chama hicho Bw. Chris Kimanga. Msafara huo
uliojumlisha zaidi ya wanachama hamsini, wakiwa wamebeba bango la chama,
ulisonga hadi kituo cha magari kwa mwendo usiokuwa wa kasi, kabla ya kupiga kona
kuelekea Magharibi hadi kituo cha ukuzaji miche, maarufu kama ‘Moi University Nursery’, karibu na soko
la wazi la ‘Mabbs’.
Ni katika kituo hicho ambapo
miche zaidi ya 500 ilipatikana, pamoja na majembe ya kupandia. Kulingana na Bw.
David Mitei ambaye ni mmoja wa wasimamizi wa kituo hicho, jamii jirani imekuwa
ikinufaika pakubwa na shughuli za kituo hicho. Kwa mfano, taasisi mbali mbali
za karibu (kama vile shule na makanisa) zimekuwa zikiwahi miche bila malipo,
hii yote ikiwa ni juhudi ya kuyaimarisha mazingira.
Kutoka hapo wanachama wa Msalaba
Mwekundu walielekea hadi maeneo ya Hosteli L, ambapo walianza kwa kuipanda miti
hiyo ili kujaliza mapengo yaliyoachwa baada ya baadhi ya miti iliyopandwa awali
kunyauka au kutonawiri ipasavyo. Baadaye walitapakaa kwengineko, kulikoonekana
na uhitaji wa miti, zikiwemo laini za kando ya kibarabara kinachounganisha eneo
hilo na Hosteli za Soweto.
Iliyodhaniwa kuwa kazi rahisi
ilipevuka upesi na kuwa ngumu na ya kuchokesha, kwani wanachama hao
walilazimika kufanya kazi kwenye miale ya jua; kunyosha kamba, kupima hatua
sita sita huku wakiweka alama, kuchimba mashimo, kuzika miche na kufunika. Ni
shughuli iliyohitaji ushirika, bidii na uvumilivu kwa zaidi ya masaa matatu
mfululizo kabla ya kufikia tamati mwendo wa saa nane mchana.
Hatimaye uliwadia ule wakati wa
kurudisha nguvu mwilini, ambapo idadi ya wanachama iliongezeka ghafla hadi
zaidi ya sabini. Walishirikiana katika riziki nyepesi iliyojumlisha soda ndogo,
thuluthi ya mkate wa boflu na pipi mbili kila mmoja kabla ya kufumukana.

