Iwapo kuna siku ya hivi karibuni ninayoingojea kwa
hamu na ghamu katika chuo hiki, si nyengine bali ni tarehe sita mwezi ujao wa
Septemba. Tukio ambalo ninalitarajia kwa
matamanio makubwa, linaloufanya moyo wangu ukose subira, ni lile la uchaguzi.
Siku hiyo kulingana na ninavyoitabiria, itakuwa
muhimu na iliyosheheni shughuli chungu nzima. Nikiwa miongoni mwa maelfu ya
wanagenzi wa chuo hiki cha Moi bewa kuu, nitaahirisha shughuli zote ambazo
ningepania kuzitekeleza siku hiyo hata kama ni kwa muda tu, ili kuitumia fursa
hiyo kuwachagua viongozi wapya watakaoshikilia nafasi mbali mbali katika
uongozi wa muungano wa wanafunzi.
Sababu kadhaa zinanishawishi na kuifanya shughuli
hiyo ya uchaguzi kuwa yenye umuhimu mkubwa katika maisha yangu kama mwanafunzi
wa chuo hiki. Kwanza ni haki ya kidemokrasia. Ikiwa kilio changu cha chini kwa
chini kila uchao, cha kutaka haki nyenginezo za msingi kama vile maisha bora
kitaendelea kugonga mgongo wa kobe, basi hii nina uhakika wa kuifurahia kwani
ni haki isiyohitaji kilio kuipata. Hakuna ajuaye, pengine nitakayemchagua siku
hiyo ndiye mkombozi aliyetabiriwa na Yohana mbatizaji na manabii wa kale kwamba
atakuja kuniondolea masaibu ya muda.
Pili ni kwamba ninahitaji kutawalwa na kiongozi ninayemuenzi,
niliyemkabidhi mamlaka mwenyewe kupitia kura yangu. Iwapo nitaamua kulipa
kisogo zoezi la uchaguzi, uamuzi huo usio wa busara hautakuwa na manufaa yoyote
kwangu, ila utafananishwa na kujitemea mate usoni mwangu mwenyewe. Nishiriki au
nisishiriki, viongozi sharti watachaguliwa na kuanza kazi mara moja. Hapo ndipo
nitakapojigundua kumbe mimi ni mtu ‘hivi hivi’, jambo ambalo siku zote nitaishi
kujutia hasa viongozi hao watakapoanza kwenda fyongo na kutoyashughulikia
maslahi yangu kikamilifu, kinyume na matarajio yangu. Hata ikiwa watafanya
vizuri, pia sitakuwa na chochote cha kujivunia kwa ajili yao, nikizingatia
kwamba sikuhusika kivyovyote katika kuwachagua.
Kwa mantiki hiyo basi siwezi kamwe kukosa kuivaa
mzima mzima shughuli hiyo ijayo ya kukata na shoka. Ikiwa sababu zote hizo
hazitoshi, naweka nadhiri ya kuziongeza wakati mwengine. Cha msingi ni kwamba naisubiri
siku hiyo kama nilivyoisubiri ile ya tarehe nne mwezi Machi mwaka huu. Swala la
iwapo zoezi zima litaendeshwa kwa njia ya kielektroniki au la; kwa foleni au
kupitia mtandao; kwa muda mrefu au mfupi; hayo si majukumu yangu. Nina imani na
maafisa wa tume huru ya uchaguzi wanaotazamiwa kutajwa hivi karibuni kwamba
watalivalia njuga swala zima na kuandaa uchaguzi wa aina yake. Ninachoomba mimi
ni uchaguzi uwe wa haki na uwazi jinsi ule wa uraisi ulivyodaiwa kuwa.
Kwa sasa nimeamua kutia masikio nta na kuzifanya
zipite juu ya hewa, tetesi kwamba mikutano ya kikabila imeanza kushuhudiwa yenye
malengo ya kusimamisha wagombea kwa misingi ya kikabila. Ninachofahamu fika ni
kwamba kiongozi yeyote atakayechaguliwa lazima atatoka katika kabila fulani
lolote lile. Hivyo basi, nimejifunza tangu utotoni kutojisumbua na wasiwasi wa
aina yoyote wa kikabila, kijinsia au kimaeneo kwani binadamu wote ni sawa mbele
za Mungu na yeyote anaweza kutunukiwa zawadi ya uongozi. Isitoshe, ninaotaka ni
uongozi bora na utapatikana tu ikiwa viongozi watakuwa bora. Je, si wale wa
kabila fulani ndio wanaojua ni mtu yupi wao aliye bora?
Hatimaye ninaelekeza dua kwa mwengezi Mungu azidi
kunineemesha neema ndogo-ndogo na neema kubwa-kubwa, niweze kuendelea kupumua kwa
pumzi yake mwenyewe hadi siku hiyo ya tarehe sita. Pia nawaombea baraka viongozi
wote wanaoondoka mamlakani na kheri njema maishani mwao pindi watakapostaafu
rasmi. Waendeleze talanta zao za uongozi walizoonyesha wakiwa madarakani kwa
muda huo mrefu mno kulingana na katiba ya uongozi. Lakini zaidi ya yote mie nitazidi
kushikilia tisti msimamo wangu wa kuisubiri siku hiyo!
